Habari

Rudi kwenye habari

JE WANAWAKE KUENDELEA KUCHOMOZA KATIKA SAMIA KALAMU AWARDS?

28 Mei 2026

Ushindani kwenye Samia Kalamu Awards unazingatia ubora na si jinsia, wanahabari wanawake wahimizwa kushindanisha kazi zao.

NI KWELI kwamba wanawake katika sekta ya habari hapa nchini wameendelea kufanya vizuri katika maeneo mbalimbali kama vile uandishi wa habari, utayarishaji wa vipindi na eneo la upigaji picha.

Samia Kalamu Awards mwaka 2025 ilipokea kazi kazi za kihabari 1,131 na baada ya majaji kuzipitia na kuzichuja kulingana na vigezo vilivyokuwa vimewekwa, washindi 43 walipatikana ambao walitokana na kazi za ki sekta, za vyombo vya habari, afisa habari bora wa serikali, Tuzo maalum na Tuzo ya ubobevu.

Wanahabari 43 waliibuka kidedea, huku 11 wakiwa ni wanawake. Hatua hii inaendelea kuleta hamasa miongoni mwa wanahabari wanawake hasa wale wanaochipukia, kwakuwa ushindani kwenye tuzo hizi ni wa wazi unaozingatia ubora wa kazi badala ya jinsia.

Washiriki wa Tuzo hizo wamekuwa wakishindana katika mazingira sawa, ambapo kazi bora ndiyo inayozungumza. Hali hiyo imeongeza kujiamini kwa wanawake wengi katika vyumba vya habari na kuwapa motisha ya kuingia zaidi katika uandishi wa habari za maendeleo, sekta ambayo kwa muda mrefu ilihitaji sauti nyingi zaidi za wanawake.

Mbali na ushindani wa haki, Tuzo za Samia Kalamu zimeanza kujenga kizazi kipya cha waandishi wanawake wenye maono ya kutumia kalamu zao kama nyenzo ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

“TAMWA tukiwa miongoni mwa waandaaji wa tuzo hizi, tunafarijika kuona idadi ya kuvutia ya wanahabari wa kike ambao wanashiriki kushindanisha kazi zao, naamini idadi yao itaongezeka kila mwaka hasa ukizingatia kwamba kwa sasa waandishi wa habari wa kike wamesambaa kote nchini” Kauli ya Joyce Shebe, aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania TAMWA, ambaye sasa amemaliza muda wake.

Aidha, waandishi wa habari wanawake wamekumbushwa kuwa Samia Kalamu Awards ni tuzo endelevu zinazolenga kukuza uandishi wa habari za maendeleo nchini.

Kutokana na hilo, waandishi wa habari wanawake wanapaswa kujitokeza kwa wingi kushiriki na kuwania tuzo mbalimbali, hususan zile za kisekta ambazo zimekuwa zikitoa nafasi kubwa kwa waandishi kuonesha ubobezi na umahiri wao.

Ushiriki wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kama mmoja wa waandaaji wa tuzo hizo pia umetajwa kuwa ishara muhimu ya dhamira ya kuhakikisha wanawake hawabaki nyuma katika safari ya kukuza taaluma ya habari nchini.

Katika dunia ya habari inayobadilika kwa kasi, wanawake waandishi wa habari sasa wanahimizwa kuamini uwezo wao, kuandika kwa ujasiri na kutumia kalamu zao kama chombo cha kuhamasisha maendeleo, kuwajibisha jamii na kuleta matumaini kwa vizazi vijavyo.

Mamlaka ya Mawasiliano nchini TCRA kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania TAMWA, waliamua kuja na tuzo hizi (Samia Kalamu Awards) ili kuhamasisha ongezeko la maudhui ya ndani ( local content) kwenye vyombo vya habari ikiwemo vya mtandaoni, kuhamasisha uandishi wa habari za maendeleo kwa kuangazia changamoto za wananchi na hatua zinazochukuliwa kutatua changamoto hizo, kufanya uchambuzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayofanyika nchini sambamba na kuhimiza weledi na matokeo chanya ya kazi za waandishi wa habari.

Picha (2)