Simulizi zinazobainisha nguvu ya kalamu kwa mwandishi aliyeitumia kalamu hiyo kwa weledi na kuleta matokeo chanya kwa jamii
Kwa miaka mingi, waandishi wa habari wamekuwa wakisimulia changamoto na mafanikio ya wananchi kupitia kalamu na kamera zao. Lakini kwa washindi wa Tuzo za Habari za Maendeleo za Samia Kalamu Awards 2025, wanakiri kwamba tuzo hizo ni mabadiliko halisi ya maisha yao binafsi na jamii inayowazunguka.
Mackriner Siyovelwa, ni mwandishi wa Crown Media, ambaye mshindi wa Sekta ya Uchumi wa Buluu, anasema ushindi huo umefungua ukurasa mpya wa mafanikio ya kitaaluma na kiuchumi maishani mwake. Anasema tuzo hizo zimempa si tu heshima katika taaluma yake, bali pia zimeongeza wigo wa mtandao wake wa wadau na fursa ndani na nje ya Tanzania.
Kupitia kazi zake zinazolenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa rasilimali za maji katika kukuza uchumi, Bi. Siyovelwa amesema sasa ujumbe wake unawafikia watu wengi zaidi kuliko alivyowahi kutarajia.
Anasema ushindi huo umeongeza kujiamini kwake kama mwandishi wa habari za maendeleo na kumfanya aamini kuwa simulizi zinazogusa maisha ya wananchi zinaweza kubadili fikra na kuchochea maendeleo ya kweli.
“Ushindi huu umenipa heshima. Zawadi kutoka SKA 2025 zimebadilisha hali yangu ya kiuchumi, lakini zaidi umenipa fursa ya kukutana na wadau wa sekta mbalimbali na kujifunza mbinu mpya za kuwasilisha maudhui yenye athari kwa jamii,” anasema Siyovelwa.
Lakini simulizi yenye kugusa zaidi inakuja kutoka kwa mshindi wa Sekta ya Maji, Bwana Adam Hhando, ambaye ushindi wake umeleta matumaini mapya katika kijiji alichozaliwa.
Hhando alipata zawadi ya shilingi milioni tano pamoja na ofa ya kuchimbiwa kisima katika Kijiji cha Changarawe wilayani Karatu, pamoja na kulipiwa gharama za maji kwa miezi kadhaa. Kwa jamii ambayo kwa muda mrefu ilikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi, zawadi hiyo imekuwa zaidi ya tuzo, imekuwa suluhisho la maisha ya kila siku.
Anasema kupitia mafanikio hayo, ameona kwa macho yake nguvu ya uandishi wa habari za maendeleo, kwamba habari zinaweza kuwa zaidi ya maneno kwenye kurasa au sauti hewani; zinaweza kuwa sehemu ya majibu ya changamoto za wananchi kama ilivyotokea katika kijiji alichozaliwa.
“Kwa mara ya kwanza nimeona nguvu halisi ya uandishi wa habari za maendeleo, siyo tu kuhabarisha, bali kuleta majibu ya changamoto za wananchi. Kisima kilichochimbwa hakinufaishi familia yangu tu, bali jamii inayotuzunguka,” amesema Hhando kwa hisia.
Kupitia Tuzo za Samia Kalamu 2025, waandishi sasa wanahamasika kufanya tafiti za kina, kufuatilia miradi ya maendeleo na kusimulia maisha ya wananchi kwa namna inayoweza kuleta mabadiliko ya kweli.
Wadau wa sekta ya habari wanaamini kuwa tuzo hizo zimekuwa chachu ya kuongeza uwajibikaji, ubunifu na ushindani wa kitaaluma miongoni mwa waandishi wa habari, huku zikitoa motisha kwa vyombo vya habari kuwekeza zaidi katika maudhui ya maendeleo.
Katika kipindi ambacho jamii inahitaji habari zenye matumaini, majawabu na dira ya maendeleo, Tuzo za Samia Kalamu zinaendelea kujijengea nafasi kama jukwaa linaloinua si tu taaluma ya habari, bali pia maisha ya watu na jamii kwa ujumla.
