Ni kicheko na tabasamu la matumaini kwa washindi wa Samia Kalamu Awards wakifungua ukurasa mpya wa maendeleo ya uchumi wao.
Washindi wa Tuzo za Habari za Maendeleo za Samia Kalamu Awards 2025 hususan mshindi Mwaka 2025 ulikuwa ni mwaka wa ujio wa Samia Kalamu Awards, hizi si tuzo zilizochagiza maendeleo na ushindani wa wanataaluma, bali ni tuzo ambazo zimetajwa kama mkombozi wa kiuchumi kwa waandishi wa habari Tanzania.
Kutoka vyumba vya habari vya magazeti, redio, televisheni na vile vya mtandaoni hadi kwa waandishi wanaotembea vijijini kusaka simulizi za maendeleo, huku weledi, ubunifu na matokeo chanya ya taarifa husika vikichagiza ushindi wa tuzo hizo.
Samia Kalamu Awards ni ufunguo wa ukurasa mpya katika taaluma ya uandishi wa habari hapa nchini. Washindi wa tuzo za mwaka 2025 wanasema wameanza kuona thamani halisi ya kuwekeza katika uandishi wa maudhui yenye kugusa maisha ya wananchi na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Baadhi ya washindi waliohojiwa wameongeza kuwa , ushindi wa tuzo hiyo haukuishia kwenye cheti na zawadi jukwaani, bali ni mwanzo wa safari mpya ya kitaaluma.
Mkurugenzi wa Televisheni wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Happiness Ngasala, ambaye chombo chake kilishinda katika kategoria ya Radio ya Kitaifa na Televisheni, anasema tuzo hizo zimeibua ushindani wa afya ndani ya vyombo vya habari na kuamsha ari mpya ya ubunifu miongoni mwa waandishi na watayarishaji wa vipindi.
Anasema sasa waandishi wengi wanatumia muda zaidi kutengeneza taarifa zinazokidhi kitaaluma , jambo ambalo linaongeza ubora wa taarifa zinazowafikia wananchi kila siku.
“Ili kushindana, wengi wameanza kuwekeza katika utafiti wa kina, matumizi ya takwimu na uwasilishaji wa maudhui yenye ushahidi. Hii inaongeza ubora wa habari zinazowafikia wananchi,” anasema Ngasala.
Ndani ya vyumba vya habari, mabadiliko hayo yanaonekana wazi. Waandishi ambao hapo awali walikimbilia taarifa za matukio ya kawaida sasa wanatafuta simulizi zinazogusa maisha ya , kuanzia changamoto za huduma za kijamii, juhudi za wananchi kujikwamua kiuchumi hadi utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.
Innocent Anselmi, mshindi wa tuzo katika Sekta ya Maliasili na Utalii ambaye pia ni Balozi wa Utalii nchini, anasema Samia Kalamu Awards zimeongeza hamasa ya kuandika habari zinazobeba matumaini, fursa na taswira chanya ya Tanzania.
Anasema kupitia tuzo hizo, waandishi wengi wameanza kuelewa kuwa habari za maendeleo zina nguvu kubwa ya kuhamasisha jamii, kuvutia uwekezaji na hata kukuza sekta muhimu kama utalii. “Waandishi sasa wanaelekeza nguvu katika kuibua masuala yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, badala ya kuishia kuripoti matukio pekee,” anasema.
Mbali na kukuza ubunifu, tuzo hizo pia zimeanza kubadilisha mtazamo wa jamii na wadau kuhusu taaluma ya habari.
Mkurugenzi wa Dodoma Media Group, Leila Sanga, anasema utambuzi unaotolewa kupitia Samia Kalamu Awards umeongeza heshima kwa vyombo vya habari na waandishi wake, huku ukiimarisha uaminifu kwa wadau mbalimbali wakiwemo watoa matangazo.
Kwa mujibu wa Bi. Sanga, kampuni nyingi sasa zinaanza kuona thamani ya kushirikiana na vyombo vinavyozalisha maudhui yenye ubora, weledi na athari chanya kwa jamii kwakuwa ndivyo vinavyofuatiliwa zaidi.
Katika mazingira ambayo dunia ya habari inabadilika kila siku, Samia Kalamu Awards zinaonekana kuwa si tu zawadi kwa washindi, bali ni uwekezaji wa moja kwa moja katika mustakabali wa uandishi wa habari za maendeleo nchini Tanzania, yaani uandishi unaosimulia maisha ya wananchi, changamoto zao, mafanikio yao na safari yao ya maendeleo.
