Napenda kuwajulisha kuwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), tumeanza maandalizi ya utoaji wa Samia Kalamu Awards (SKA) 2026 ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan
Dar es Salaam, Aprili 2026
Ndugu waandishi wa habari,
Habari za asubuhi,
KAZI na UTU,
Napenda kuwajulisha kuwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), tumeanza maandalizi ya utoaji wa Samia Kalamu Awards (SKA) 2026 ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kama mtakumbuka, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Katika hotuba yake ya ufunguzi rasmi wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 14 Novemba, 2025, alibainisha dhamira ya Serikali anayoiongoza kuendelea kutambua mchango wa waandishi wa habari za maendeleo nchini kupitia Samia Kalamu Awards (SKA). Tamko hilo pia ni mwendelezo wa ahadi aliyoitoa wakati wa hafla ya utoaji tuzo hizi Mei, 2025.
Mhe. Rais alielekeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na wadau wengine kuendelea kuratibu na kuunga mkono utoaji wa tuzo hizi kila mwaka.
Ili kuhakikisha uadilifu, uwazi na ushindani wa haki, maandalizi ya tuzo hizi yanahusisha pia Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kama mdau muhimu katika kusimamia weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari, kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari (2016).
Tuzo hizi zinalenga kutambua, kuthamini na kuhamasisha uzalishaji wa maudhui ya ndani yenye ubora, yanayochangia kuelimisha, kuhabarisha na kuburudisha, na kuimarisha taswira chanya ya Taifa, kupitia habari za maendeleo.
Tangu kuanzishwa kwa SKA mwaka 2025, tuzo hizi zimekuwa kichocheo muhimu cha kuhamasisha uandishi na uandaaji wa habari na makala zinazozingatia utafiti na uchambuzi wa kina wa masuala ya maendeleo, uwajibikaji, uzalendo na ujenzi wa taswira chanya ya Taifa.
Katika awamu ya kwanza, tuzo hizi zilipata mwitikio mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali wa sekta ya habari, zikiwemo taasisi za habari, waandishi wa habari binafsi watayarishaji wa Maudhui mtandaoni, na maafisa habari wa Serikali.
Awali TCRA na TAMWA tuliendesha mafunzo ambapo zaidi ya waandishi wa habari 2,000 walinufaika na mafunzo maalumu yaliyolenga kukuza uandishi wa habari za maendeleo, hatua iliyochangia ongezeko la maudhui ya ndani yenye ubora na tija kwa jamii.
Kwa mwaka 2026, tumejipanga kuendeleza mafanikio haya kwa kuhakikisha kuwa, tuzo hizi zinaendelea kuwa jukwaa madhubuti la kuibua na kutambua kazi bora za uandishi wa habari zinazochangia maendeleo ya Taifa.
Samia Kalamu Awards (2026) itahusisha makundi yafuatayo:
(i) Tuzo Maalumu za Kitaifa.
(ii) Tuzo kwa Vyombo vya Habari.
(iii) Tuzo za Kisekta.
Maelezo zaidi kuhusu makundi na vigezo, tembelea tovuti: samiaawards.tz
C. VIGEZO VYA JUMLA VYA USHIRIKI
MWANDISHI WA HABARI
(i) Awe raia wa Tanzania;
(ii) Awe amethibitishwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kwa upande wa Tanzania Bara, kwa Zanzibar awe na kitambulisho cha mwandishi wa habari (Press Card);
(iii) Asiwe na rekodi ya kutiwa hatiani kwa kosa lolote la jinai;
KAZI INAYOWASILISHWA
(i) Iliyochapishwa, kutangazwa au kurushwa kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza katika vyombo vya habari vya ndani au nje ya Tanzania;
(ii) Iliyofanyiwa utafiti wa kina, inayohusisha uchambuzi na takwimu;
(iii) Inayohusisha vyanzo vya habari visivyopungua vinne (4);
(iv) Haijashindanishwa katika tuzo nyingine;
(v) Imechapishwa, kutangazwa au kurushwa kati ya Julai 01, 2025 hadi Juni 15, 2026;
(vi) Inayohusu masuala ya maendeleo na kuibua simulizi za wananchi zinazoonesha namna miradi ya kitaifa ilivyofungua fursa na kubadili maisha ya wananchi;
(vii) Iwe na maudhui yanayozingatia ulinzi wa haki-miliki na haki shiriki;
CHOMBO CHA HABARI
(i) Kiwe na leseni hai iliyotolewa na mamlaka husika.
Mchakato wa kupokea kazi utaanza rasmi leo tarehe 31 Mei 2026 na kuhitimishwa tarehe 30 Juni 2026 kupitia tovuti ya tuzo ambayo ni samiaawards.tz. Kazi zitakazopokelewa ni zilizochapishwa au kurushwa kuanzia tarehe Moja Julai 2025 hadi tarehe 30 Juni 2026.
Tunahimiza waandishi wa habari na vyombo vya habari Tanzania bara na Zanzibar kuwasilisha makala za maendeleo kwa wakati. Kazi zitakazowasilishwa zitafanyiwa tathmini na jopo huru la majaji wenye ubobevu katika taaluma ya uandishi wa habari, uhusiano na mawasiliano kwa umma. Kazi zote ziwasilishwe kupitia tovuti ya samiaawards.tz
Kazi zitakazopitishwa na majaji zitapigiwa kura na wananchi kupitia tovuti ya samiaawards.tz au kupitia ujumbe mfupi wa simu(SMS)
Ili kuhakikisha kunakuwa na uwiano kati ya weledi wa kitaaluma na maoni ya hadhira/wananchi majumuisho ya kura yatahusisha:
(i) Kura za wananchi zitachangia asilimia 60
(ii) Majaji watachangia asilimia 40
Mfumo huu unalenga kuhakikisha washindi wanatambuliwa kwa kuzingatia ubora wa kazi pamoja na namna kazi hizo zinavyoathiri maendeleo ya wananchi na uchumi wa taifa letu.
Tunatarajia tuzo hizi zitatolewa kati ya mwezi Oktoba na Desemba 2026.
TCRA na TAMWA tunaamini kuwa Samia Kalamu Awards zitaendelea kuwa chachu muhimu ya kuendeleza taaluma ya uandishi wa habari nchini kwa kuhamasisha uzalishaji wa maudhui yenye ubora, yanayozingatia maadili, weledi na yenye mchango chanya katika maendeleo ya Taifa.
Hivyo basi, tunawahimiza waandishi wa habari na watengenezaji wa maudhui kote nchini kushiriki kikamilifu katika tuzo hizi kwa kuwasilisha kazi zenye ubora, ili kwa pamoja tuendelee kukuza uandishi wa habari wenye tija kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Imetolewa na:
Mha. Peter P. Mwasalyanda
MWENYEKITI , Samia Kalamu Awards (SKA)
Dkt. Rose Reuben
MWENYEKITI MWENZA, Samia Kalamu Awards (SKA)
Asanteni kwa kunisikiliza!.
